Dkt. Mzee Suleiman Mndewa
PhD in Optoelectronic Information Engineering
Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari yameleta mageuzi makubwa katika maisha ya mwanadamu pamoja na maendeleo yake kwa ujumla , hivi leo tunashuhudia kuona matumizi ya Tehama yanavotumika ili kukuza uchumi katika mataifa mbali mbali duniani . Matumizi ya Tehama yanapunguza gharama katika uzalishaji , utoaji huduma na uendeshaji katika sekta mbali mbali za kiserikali pamoja na za kijamii, hivyo basi hatuna budi kujifunza na kutumia fursa hiyo ili kujiletea maendeleo pamoja na kuondoa umaskini. Halikadhalika TEHAMA hivi leo inatumika katika sekta za elimu, sekta za afya ili kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo. Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi za makusudi imejenga miundombinu ya mawasiliano ya mkonga ili kuboresha huduma za mawasiliano hapa Zanzibar. Hivyo basi miundombinu hiyo ni muhimu kulindwa ili isije ikahujumiwa na kusababisha kuzorota kwa huduma za mawasiliano nchini kwani miundombinu hiyo huchangia shughuli za kiuchumi pamoja na zile za kijamii kutoka Zanzibar kwenda duniani kote kwa kupitia mkonga wa kimataifa.